Tangazo

Bongo Flava ya Sasa ni chai ya Moto Ukinywa lazima Upulize

Muungwana lazima nilonge maana maji yamenifika Hapaaa. Yawezekana nikaonekana kipofu mbele yako ama kuonekana mtu wa kale ila kiukweli mimi ni sawa na mvinyo wenye umri mkubwa katika chupa ya mchungaji wa kondoo nyikani.

Kwa muda mrefu nimekua mshabiki na mdau mkubwa sana wa muziki wetu huu wa bongo flava, tangu kuanza kwake nimekua nauna na yawezekana hata kufa kwake nitashuhudia maana siku sii nyingi zilizobakia kufa kwake.

Nachomaanisha mimi ni kwamba muziki wetu huu umebadilika mno tena sana. Ni wazi kwamba ni lazima mambo yabadilike ili kuendana na Nyakati zilizoko, Lakini Uhalisia wa mambo hayo lazima ubaki pale pele(Ndivyo ilivyo siku zote na ndio maana wewe ni yule yule wa tangu kuzaliwa kwako ila Umekua na kubadilika).

Ilichukua muda mrefu na Nguvu kubwa kuianzisha na kuiendeleza Bongo flava na ndio maana watu weengi walikua wakishindwa kuutambua muziki huu ni wa aina gani ila baadae waliutambua na kuupenda mara dufu, Vipaji vya kweli vilikuwako na hapa nazungumzia waandaji(Producers) na Wasanii.

Ladha na Utamu wa Bongo flava ya kipindi kile niliifananisha na Wali nazi yaani utamu wake asikunyime mtu ila sasa napata wakati mgumu kuipata ile ladha ya wali nazi naishia kupata ladha ya maji ya Kunywa.

Sii kwa Producers wala kwa wasanii kwa ujumla, Iko wapi ile mikono ya P Funk Majani, Master J, Mwika Mwamba, Endrico na Kina Dunga? Wako wapi wasanii wetu Dojo na Domo Kaya, Daz Baba na Daz Nunda, wakina Dataz? Yako wapi Makundi makubwa yaliyojawa na Haiba kama East Coast Team, Manduli Mob, solid Ground, Watengwa na Wakali Kwanza? – Kiukweli nimeyakumbuka mengi na nayakosa mambo hayo.

Sisemi kwamba Bongo Flava ya sasa haina watu wa aina hiyo, laa hasha, nachomaanisha mimi ni kwamba Wasanii na Producers wa sasa hawaitendei haki ile Bongo Flava ya zamani na badala yake wamekua wakiiga miziki ya wenzetu huko Ughaibuni. Inafika pahala unashindwa kuutofautisha Muziki wa Sasa na Muziki wa Nigeria ama Africa Kusini. Mikono ya Producer Huyu na Yule ihaina tofauti hata kidogo. Ubunifu na Utunzi wa sasa ni kiwango cha chini Mno, zile jumbe tulizokua tukizipata katika Bongo Flava ile kwa sasa haupo tena.

Inanipa wakati mgumu kuusikiliza Bongo Flava ya sasa na ndio maana nasema Bongo Flava ya sasa ni chai ya Moto

AdvertisementMtokambali 728x90