Tangazo

Sura hii inajadili njia mbalimbali za kuzuia mimba au kupanga muda wa kupata mimba nyingine yaani Uzazi wa mpango. Njia zote ambazo zimeelezewa katika sura hii hutumika sehemu zote duniani.

Kwa nini uzazi wa mpango?

Kuna njia nyingi salama na zenye uhakika za kuzuia mimba, au kukusaidia kuchagua lini upate mtoto na idadi ya watoto ungependa kuzaa. Unaweza kupata njia za kuzuia mimba zenye gharama nafuu au zisizo na malipo kabisa kutoka kliniki za uzazi wa mpango katika mazingira yako ya kawaida. Uzazi wa mpango hujulikana pia kama kama njia ya kudhibiti uzazi. Haijalishi maneno gani ambayo yanatumika, uzazi wa mpango una manufaa mengi:

 • Kuzaa idadi ndogo ya watoto ni bora zaidi kwa afya ya mwanamke kuliko kuzaa watoto wengi. Kwa kutumia njia ya uzazi wa mpango, unaweza kuamua lini mwili wako uko katika hali nzuri kiafya kubeba mimba.
 • Kuvuta subira katika uzazi na kuacha muda wa kutosha kati ya mtoto mmoja na mtoto mwingine hukuwezesha kuwaandalia watoto utakaowazaa maisha ya uhakika, na kukupa muda zaidi, nguvu, na fedha kwa ajili ya kuwahudumia watoto ambao tayari unao.
 • Kuamua kama unataka kupata watoto na lini, bila watu au mtu mwingine kukuamrisha kupata mimba au usipate mimba: kuchukua hatamu ya maisha yako.
 • Kufurahia tendo la kukutana kimwili bila kuwa na wasiwasi wa kupata mimba kama wewe na mwenzako hamtaki au hamjawa tayari kupata mtoto.
 • Uzazi wa mpango huwasaidia wanawake kuepuka utoaji mimba usiyo salama, tatizo ambalo husababisha vifo vya maelfu ya wanawake kila mwaka.

Uzazi wa mpango, tendo la ngono, mimba — wakati mwingine ni mambo magumu kuyazungumzia. Kitabu cha Hesperian kijulikanacho kama Juhudi za afya kwa wanawake (Health Actions for Women) kimependekeza njia za kuwawezesha wanaume na wanawake kuuzungumzia uzazi wa mpango na masuala mengine ya afya ya wanawake.

Baadhi ya watu hupenda kuzaa watoto wengi-hasa watu wa kawaida na mara nyingi wenye hali duni (baadhi ya watoto kufariki wakiwa wadogo) kwa sababu watoto husaidia kufanya kazi na kuwatunza wazazi wao wanapozeeka.

Uzazi wa mpango
Uzazi wa mpango

Hali ni tofauti katika nchi zenye mgawanyo mzuri wa rasilimali na manufaa yatokanayo. Mahali ambapo ajira, makazi, na huduma za afya vinapatikana kwa urahisi zaidi, na mahali ambapo wanawake wana fursa sawa na wanaume kielimu, ajira, na katika kuendesha maisha yao, watu mara nyingi huchagua kuwa na familia ndogo. Sababu ni kwamba, kwa kiasi fulani, hawahitaji kuwa tegemezi kwa watoto wao kiuchumi, na wana imani kubwa zaidi kuwa watoto wao wataishi maisha bora kiafya, kijamii na kiuchumi.

Watu hutumia njia za uzazi wa mpango ikiwa:

 • Inatolewa kwa gharama nafuu au bila malipo.
 • kuna njia za uzazi wa mpango tofauti ili watu waweze kuchagua njia ipi inayowafaa.
 • hakuna mtu anayeshinikizwa au kulaghaiwa kutumia njia hiyo ya uzazi wa mpango.
 • wanaume wanaelewa na kuamini manufaa ya uzazi wa mpango, na kuwasikiliza wanawake wanachotaka.
 • mtu yeyote ambaye anataka kutumia uzazi wa mpango anaweza kuipata huduma hiyo kwa urahisi, wakiwemo vijana au watu wazima, ambao wameolewa na hawajaoa au kuolewa, na watu wenye ulemavu.

  Uzazi wa mpango ni kwa ajili ya nani ?

  Uzazi wa mpango
  Uzazi wa mpango ni kwa ajili ya yoyote ambaye anaweza kupata mimba-lakini hataki kupata mimba kwa wakati huo.

  Baadhi ya watu hufikiri kuwa uzazi wa mpango ni kwa ajili ya wanawake walioolewa tu. Lakini wanawake wengi ambao wameoolewa na hawajaolewa hufanya tendo la ngono, na wengi wanataka kufurahia tendo hilo bila kuwa na wasiwasi au uoga wa kupata mimba. Vilevile, wanawake mara nyingi huwa hawana maamuzi ya mwisho juu ya tendo la ngono. Baadhi hushinikizwa au kulazimishwa. Hata hivyo, bila uzazi wa mpango, mwanamke yeyote, aliyeolewa au hajaolewa, mwenye umri mdogo au mkubwa, anaweza kupata mimba. Ukiwa mfanyakazi wa afya au katika nafasi yotote ya uelimishaji, ni muhimu kueneza elimu ya uzazi wa mpango kwa wanawake wote.

  Uzazi wa mpango

  Unapaswa pia kutafuta njia za kuwapa elimu wanaume juu ya uzazi wa mpango. Baadhi ya njia za uzazi wa mpango, mfano kondomu, huhitaji azma ya wanaume. Na mara nyingi mwanaume hutarajiwa kuchangia uamuzi juu ya njia ya uzazi mwenzi wake atakayoitumia. Kuwasiadia wanaume kuelewa manufaa au faida za uzazi wa mpango huwasaidia kuondokana na wasiwasi wao juu ya njia husika na kuelewa jinsi uzazi wa mpango unavyowasaida pia.

  Kuwapa elimu wanaume juu ya uzazi wa mpango pia humrahihishia mwanamke kuongea na mume au mwenzi wake juu ya uzazi wa mpango na na kuamua njia ipi watumie. Kama mwanaume bado hataki kutumia uzazi wa mpango hata baada ya kujifunza na kuelewa faida zake, mwanamke atahitaji kuamua iwapo anapaswa kuendelea kuitumia katika hali kama hiyo. Kuna njia ambazo mwanamke anaweza kutumia bila mwanaume kujua.

  Elimisha jinsi njia za uzazi wa mpango zinavyofanya kazi na nini cha kutarajia

  Elezea jinsi ya kutumia njia mbalimbali za uzazi wa mpango kwa usahihi na kuwa mkweli juu ya madhara yake ya pembeni. Sababu kuu ya wanawake kuacha kutumia njia ya uzazi wa mpango ni kutokana na kero ya madhara yake ya pembeni. Lakini kama atajua mapema juu ya madhara hayo, anaweza kuwa tayari kuendelea na njia hiyo hadi madhara yatakapopungua au kuachagua njia nyingine inayomfaa zaidi.

  Kuwasaidia vijana

  Vijana wanaweza kuanza mahusiano ya kimapenzi au hata kingono kabla hawajajua jinsi ya kuzuia kupata mimba. Jamii zinaweza kuwasaidia vijana kupata taarifa ambazo wanahitaji ili kufanya maamuzi sahihi. Shule zinaweza kuwapatia vijana elimu ya afya ambayo inajumuisha suala la mimba. Vijana pia wanaweza kufundishwa kuwa walelimishaji rika na muda maalum unaweza kupangwa kwenye kliniki na sehemu zingine ili kuwapatia vijana unasihi na nyenzo za kuzuia mimba.

  Jinsi mwanamke anavyopata mimbaUzazi wa mpango

  Uzazi wa mpango

  Mwanaume anapofikia kilele na kuachia shahawa ndani au karibu na uke, shahawa kutoka kwenye ume huingia kwenye mji wa mimba au kizazi cha mwanamke na kwenye njia za kusafirisha mayai ya kike ya uzazi. Kama ni wakati wa kipindi cha rutuba(kipindi cha mwanamke kushika mimba), mbegu ya kiume inaweza kuungana na yai la kike lililopevuka. Kama mbegu ya kiume itarutubisha yai hilo, basi hujibanza kwenye ukuta wa mji wa mimba(kizazi). Hapo mimba itakuwa imetunga. Njia za uzazi wa mpango huzuia mimba kwa kuzuia mbegu za kiume kuingia kwenye uke, au kusimamisha mwili wa mwanamke usiachie mayai ya uzazi, au kuzuia mbegu za kiume kukutana na yai.

 • Soma pia:Ujauzito na kujifungua; Jinsi ya kuendelea kuwa na afya bora wakati wa ujauzito.

   Njia za uzazi wa mpango

  Sura hii inaelezea njia tofauti za uzazi wa mpango. Kwa ajili ya taarifa juu ya njia zingine za uzazi wa mpango, na zile ambazo hazitumiki sana.

  Jinsi ya kuchagua njia ya uzazi wa mpango

  Njia zote tofauti za uzazi wa mpango zina manufaa na mapungufu. Ni muhimu kuongea na mwenzi wako, wanawake wengine, au mfanyakazi wa afya juu ya njia tofauti kukusaidia kuchangua njia inayokufaa. Baadhi ya mambo ambayo unatakiwa kuzingatia katika kuchagua njia ya uzazi wa mpango ni pamoja na:

  • Ina ufanisi kiasi gani katika kuzuia mimba?.
  • Ina ufanisi kiasi gani katika kukinga dhidi ya magonjwa ya ngono?.
  • Kama mwenzi wako anaafiki matumizi ya njia hiyo ya uzazi wa mpango, au kama unapaswa kuficha asijue.
  • Kama njia hiyo inapatikana kwa urahisi, na mara ngapi unatakiwa kiutumia katika muda fulani.
  • Inagharimu kiasi gani ?.
  • Kama ina madhara ya pembeni.
  • Kama una mahitaji na wasi-wasi mwingine. Kwa mfano: unanyonyesha? Bado unahitaji watoto zaidi ?
  Una haki wewe mwenyewe kufanya maamuzi yanayohusu uzazi wa mpango.
  NJIA YA UZAZI WA
  MPANGO
  Uwezo wa
  kuzuia
  mimba
  Uwezo wa
  kukinga
  dhidi ya
  maambukizi
  kupitia
  ngono
  Matumizi
  yake
  Maelezo mengine muhimu
  Kondom

  Mkubwa Mkubwa zaidi Wakati wote Hufanya kazi kwa ufanisi zaidi inapotumika na dawa ya kuua mbegu za kiume na kilainishi cha asili ya maji. Kondom hutakiwa kutumika kila mara unapofanya tendo la ngono.
  Vidonge vya majira-Vidonge mseto

  Mkubwa sana Sifuri Kila siku Hufanya kazi vizuri zaidi inapotumika muda ule ule kila siku. Wanawake wenye matatizo ya kiafya yafuatayo hawapaswi kutumia njia hii.
  Vidonge vya majira (vyenye homoni moja-siyo mseto)

  Mkubwa sana Sifuri Kila siku Hufanya kazi pale tu inapotumiwa saa ile ile kila siku. Inaweza kutumiwa hata na wanawake wanaonyonyesha (anza angalau baada ya mtoto kufikisha wiki 6).
  Vijiti

  Mkubwa zaidi Sifuri Miaka 3 hadi 5 Lazima vingizwe na kutolewa na mfanyakazi wa afya ambaye amepitia mafunzo maalum na kubadilishwa kila baada ya miaka 3 au 5 kutegemea na aina ya vijiti.
  Sindano

  Mkubwa sana Sifuri Mwezi 1, 2, au 3 Inatakiwa kurudiwa kila baada ya mwezi 1, 2, au 3 (kutegemea na aina ya sindano).
  Kitanzi

  Mkubwa zaidi Sifuri Miaka 5 au 12 Hufanya kazi kwa muda wa miaka 5 au 12 (kutegemea na aina ). Lazima kiingizwe na kutolewa na mfanyakazi wa afya ambaye amepitia maafunzo maalum.
  Kuchomoa uume mwanaume anapofikia kileleni

  Mdogo sana Sifuri Wakati wote Mwanaume anatakiwa kuchomoa uume wake haraka anapofika kileleni kila mara mnapofanya tendo la ngono. Hata kama atachomoa uume, majimaji kidogo kutoka umeni yanaweza kuingia ukeni wakati wa tendo la ngono na kusababisha mimba kutunga, hali ambayo pia inaweza kusababisha maambukizi yanayopitia ngono.
  Unyonyeshaji (wakati wakati wa miezi miezi 6 tu ya kwanza) Mkubwa sana Sifuri Mara kadhaa mchana na usiku Njia hii hufanya kazi tu kama mwanamke ananyonyesha mtoto wake maziwa ya mama tu na kama hedhi zake hazijaanza tena.
  Njia ya kuhesabu siku (kushika mimba)

  Mkubwa Sifuri Kila mara Njia hii haifanyi kazi vizuri kwa wanawake wenye mzunguko wa hedhi unaobadilika.
  Tendo la ngono lisilohusisha uume kuingizwa kwenye uke Mkubwa zaidi Inategemea Kila mara Kama uume haugusi uke, mwanamke hawezi kupata mimba. Ngono kwa njia ya haja kubwa inaweza kusababisha maambukizi kwa urahisi. Ngono kwa njia ya mdomo ina uwezekano mdogo wa kusababisha maambukizi ya magonjwa yanayopitia ngono. Mguso tu wa kingono bila kuingiliana ni nadra kusababisha maambukizi yoyote.
  Kufunga kizazi kabisa Mkubwa zaidi Sifuri Mara moja Mara mwanamke au mwanaume anapofunga kizazi kabisa, hatabeba mimba au kusababisha mimba tena.

   

   

  SOMA HII: Nani hapaswi kutumia vidonge mseto vya majira

 • Mara nyingi watu hutumia njia tofauti kutegemea na mazingira yao.

  Kondomu

  Kondomu ni kimfuko laini chembamba ambacho mwanaume huvaa kwenye uume wake wakati wa kufanya tendo la ngono. Shahawa za mwanaume hubaki ndani ya kondomu, na hivyo haziwezi kuingia ukeni na kusababisha mimba. Kondomu ni salama na hazina madhara ya pembeni.

  Kondomu ni njia yenye uwezo mkubwa zaidi wa kuzuia maambukizi ya magonjwa ya ngono, ukiwemo VVU. Hata kama unatumia njia nyingine ya uzazi wa mpango, unaweza wakati huohuo kutumia kondomu kwa ajili ya kujikinga wewe na mwenzi wako dhidi ya magonjwa yanayoambukizwa kupitia ngono.

  Kondomu ndiyo njia pekee ya uzazi wa mpango ambayo inaweza, kwa kiwango kikubwa, kuzuia mimba na kukinga dhidi ya maambukizi kupitia ngono kwa wakati mmoja. Lakini mwanaume lazima awe tayari kutumia kondomu kila mara atakapofanya ngono.

  Minya ncha ya kondomu na kuivalisha kwa kuviringisha juu ya uume uliosimama. Ncha ya chini yenye nafasi hupokea shahawa za mwanaume baada ya kuachiwa. (Kama hutaacha nafasi kwa ajili ya shahawa, kondomu inaweza kupasuka.)

  Baada ya kufikia kileleni, ume ungali bado umesimama, shikilia kondomu kwa juu ili ibaki kwenye ume wakati ukichomoa ume kutoka ukeni. Baada ya hapo, toa kondomu kwenye ume. (Tupa kondomu kwenye chombo cha taka – usitupe kondomu hovyo ili watu wengine wasiiguse au kuiokota!) Tumia kondomu mpya kila mara unapofanya tendo la ngono.

  Kondomu ya kike

  Pete la mpira huingizwa ndani ya uke. Pete la nje hubaki nje ya uke.
  Pete la mpira huingizwa ndani ya uke. Pete la nje hubaki nje ya uke.

  Kondomu ya kike hufitishwa kwenye uke na kufunika mlango wa uke. Ni kubwa kuliko kondomu ya kiume na uwezekano wa kuvunjika ni mdogo sana. Kondomu za kike hutoa kinga dhidi ya VVU na maambukizi mengine ya ngono.Usitumie kondomu ya kiume na ya kike kwa pamoja katika tendo la ngono.

  Dawa za kuua mbegu za kiume (Spermicide)

  Dawa za kuua mbegu za kiume kwenye shahawa zinaweza kuwa katika mfumo wa povu, vidonge, mafuta ya krimu, jeli au vidonge ambavyo huyeyuka kwenye uke na kuua mbegu za kiume ili zisiweze kurutubisha yai.

  Kifaa cha kuingizia dawa

  Dawa za kuua mbegu huingizwa ukeni mara kabla ya tendo la ngono. Dawa haifanyi kazi vizuri ikitumika peke yake, lakini hutoa kinga zaidi dhidi ya mimba inapotumika pamoja na kondomu. Dawa za kuua mbegu za kiume hazitoi kinga dhidi ya maambukizi yanayopitia kwenye ngono au VVU.

  Vidonge vya kuzuia mimba (vidonge vya majira)

  Vidonge vya kuzuia mimba vina homoni ambazo zinafanana na homoni za asili kwenye mwili wa mwanamke. Huzuia mimba kwa kusimamisha ovari za mwanamke kuachia yai. Kuna aina kuu 2 za vidonge vya majira: vidonge mseto vyenye homoni 2, estrojeni na projestini, na vidonge vidogo ambavyo vina homoni moja tu ya projestini. Vidonge vya majira havitoi kinga dhidi ya VVU au maambukizi mengine kupitia ngono. Ili uweze kujilinda dhidi ya magonjwa hayo, unapaswa kutumia pamoja na kondomu.

  Baadhi ya wanawake huamua kutumia vidonge vya majira kwa sababu vidonge hivyo husaidia kuweka vizuri mpangilio wa hedhi, ili waweze kujua lini siku zao za hedhi zitaanza. Vidonge vya majira pia hupunguza wingi wa damu ya hedhi, na mabonge ya damu na maumivu wakati wa hedhi.

  Vidonge vya majira havisabishi saratani.

   

  Vidonge vya majira mseto (vyenye homoni za estrojeni na projestini)

  Aina tofauti za vidonge mseto vya majira vina dozi tofauti za homoni hizi mbili. Kuna mseto wenye dozi za kawaida kama vile miligramu 1 au chini yake ya projestini na maikrogramu 30 au 35 za estrojeni (ethinyl estradiol), au maikrogramu 50 ya estrojeni nyingine iitwayo mestranol.

  Baadhi ya vidonge vya majira vina homoni ya projestini tu.

  Vidonge vya majira hufanya kazi vizuri kuzuia mimba vinapotumika kila siku na muda ule ule. Ni salama kwa wanawake walio wengi.

  Jinsi ya kutumia vidonge mseto vya majira

  Kama una uhakika kuwa huna ujauzito, unaweza kuanza kutumia vidonge vya majira wakati wote. Vidonge vya majira havitazuia mimba hadi uwe umekua ukivitumia angalau kwa wiki. Hivyo katika siku 7 za mwanzo baada ya kuanza kutumia vidonge vya majira, tumia kondomu au epuka ngono.

  Unatakiwa kutumia kidonge 1 cha majira kila siku kuzuia mimba, hata kama hutafanya tendo la ngono siku hiyo. Jitahidi kutumia kidonge muda ule ule kila siku. Kuweka vidonge mahali unapolala, kunaweza kukusaidia kukumbuka kumeza kidonge kila siku kabla hujalala. Aina nyingi za vidonge vya majira mseto huwa katika paketi ya vidonge 28 au 21.

   

  Madhara ya pembeni ambayo yanaweza kuhusiana na vidonge mseto vya majira

  Madhara ya pembeni siyo hatari sana lakini mengine yanaweza kukera. Kawaida hupungua au kutoweka baada ya miezi 3. Wakati mwingine unaweza kujaribu aina nyingine ya vidonge vya majira.

  Mabadiliko katika hisia kama vile kuhisi huzuni au kuudhika kwa urahisi Maumivu ya kichwa Kutokwa na damu kidogo katikati ya vipindi vya kawaida vya hedhi.
  Matiti kuvimba na kuuma Kichefuchefu

  Vidongo mseto vya majira vinaweza kutumika kupitia njia 3

  Kutumia siku 28: Tumia vidonge vyenye homoni kwa siku 21 na baada ya hapo, kwa siku 7, tumia vidonge vilivyobaki. (Vidonge vya ziada kwenye paketi havina homoni), au usitumie tena vidonge. Utakuwa unapata hedhi kila mwezi wakati wa siku hizo 7 kama hedhi nyingine ya kawaida.

   
  Kama una paketi ya siku 28, tumia kidonge 1 kila siku. Vidonge 7 vya mwisho ni kwa ajili ya kukukumbusha kuwa havina homoni – Vimewekwa kukusaidia kukumbuka kutumia kidonge cha majira kila siku. Vidonge 7 vya mwisho kwenye paketi vitakuwa vya rangi tofauti.
  Kama una paketi ya siku 21, tumia kidonge 1 kila siku kwa siku 21 – paketi nzima. Basi usitumie kidonge kwa siku 7. Anza paketi nyingine.

  Matumizi ya muda mrefu: Tumia vidonge vyenye homoni kwa siku 84 vinavyofuatana na baada ya hapo pumzika kwa siku 7. Wakati mwingine vidonge huwa kwenye paketi zenye vidonge 91 (84 vyenye homoni na 7 kwa ajili ya kukumbusha tu ambavyo havina homoni). Wakati wa siku hizo 7, utakuwa unapata hedhi kama inavyokuwa katika hedhi ya kawaida lakini mara moja tu katika kipindi cha miezi 3. Matone ya damu (hedhi nyepesi sana) yanaweza kutokea lakini hutoweka baada ya miezi michache.

   

  Matumizi endelevu: Tumia vidonge vyenye homoni kila siku bila kuacha. Kama utaona usumbufu na hedhi isiyotabirika, acha kutumia vidonge kwa siku 3 au 4 ili kupata siku chache za hedhi ya kawaida, halafu endelea kutumia kidonge tena kila siku.

  Utaratibu wote huu wa kutumia vidonge mseto ni salama. Mtu yeyote ambaye anatumia vidonge mseto vya majira anatakiwa kujua afanye nini kama ataruka kemeza kidonge kimoja au viwili:

  Kama utasahau kumeza kidonge 1 au 2, tumia kidonge 1 haraka mara utakapokumbuka. Baada ya hapo tumia kidonge kinachofuata katika muda wa kawaida. Hii inaweza kumaanisha kwamba utatumia vidonge 2 katika siku moja.

  Kama utasahau kutumia vidonge 3, siku 3 zinazofuatana, tumia kidonge 1 mara moja. Baada ya hapo, tumia kidonge 1 kila siku katika muda ule ule. Tumia kondomu hadi utakapoanza hedhi yako, au usifanye ngono hadi utakapokuwa umetumia kidonge kila siku kwa siku 7 mfululizo.

  Kama hedhi yako haitakuja muda wake wa kawaida na umesahau kumeza baadhi ya vidonge, endelea kutumia vidonge vyako, lakini pata kipimo cha mimba. Kama utakuta una mimba, simamisha kutumia vidonge.

  Kusitisha matumizi ya vidonge mseto vya majira

  Unaweza kusimamisha matumizi ya vidonge wakati wote. Unaweza kupata mimba mara moja, hivyo iwapo unataka kuepuka kupata mimba, tumia kondomu au njia nyingine.

   

  Nani hapaswi kutumia vidonge mseto vya majira

  Baadhi ya wanawake wana matatizo ya kiafya na matumizi ya vidonge mseto vya majira vinaweza kuhatarisha maisha yao. Usitumie vidonge mseto vya majira iwapo:

  • Una tatizo la presha kubwa ya juu (160/110 au juu zaidi). Angalia Magonjwa ya moyo (kinaandaliwa) kwa ajili ya taarifa zaidi juu ya tatizo la Shinikizo la Presha ya Juu.
  • Ugonjwa wa kisukari kwa zaidi ya miaka 20.
  • Kama una zaidi ya miaka 35 na ni mvutaji wa sigara.
  • Tatizo la maumivu makali ya kichwa (maumivu ya kichwa makali yakiambatana na kichefuchefu) kama yakiambatana na kufa ganzi au na matatizo makubwa katika kuona.
  • Saratani ya matiti, saratani ya ini, au saratani ya kibofu cha mkojo. Angalia Saratani (kinaaandaliwa).
  • Ugonjwa wa kibofu cha nyongo.
  • Uliwahi kupatwa na kiharusi.
  • Damu kuganda kwenye mshipa (hali hii kawaida husababisha joto na maumivu kwenye mguu mmoja).
  • Ugonjwa wa ini au homa ya manjano au hepatitis.

  Wanawake wengi wenye tatizo moja la kiafya wanaweza kutumia kwa usalama vidonge vya majira vyenye projestini tu au njia ya vijiti au sindano za projestini tu. Wanawake wenye ugonjwa wa saratani ya matiti au saratani ya tumboni hawapaswi kutumia njia za uzazi wa mpango zenye homoni, na badala yake watumie njia nyingine.

  Dawa ambazo zinaingiliana na vidonge mseto vya majira

  Rifampicin (dawa ya kifua kikuu), ritonavir (dawa ya VVU) na baadhi ya dawa za kifafa huathiri utendaji wa vidonge vya majira. Kama utatumia dawa hizi, chagua njia tofauti ya uzazi wa mpango. Wanawake wanaotumia insulini kwa ajili ya kisukari wanaweza kuhitaji kurekebisha kiasi cha insulini baada ya kuanza kutumia vidonge vya majira.

  Nani wanapaswa kufikiria njia zingine kama zipo

  Kuna matatizo machache ya kiafya ambayo hufanya njia ya vidonge vya mseto vya majira kutofaa baadhi ya watu. Ni bora zaidi kwa wanawake wenye matatizo haya kutumia njia nyingine ya kupanga uzazi:

  • Tatizo la shinikizo la juu la damu-presha ya juu (zaidi ya 140/90). Angalia Ugonjwa wa moyo (kinaandaliwa) kwa taarifa zaidi juu ya shinikizo la juu la damu.
  • Kama una zaidi ya miaka 35 na una matatizo ya kuumwa kichwa (maumivu ya kichwa yanayoambatana na kichefuchefu).

  Kama mwanamke mwenye matatizo atatumia vidonge mseto vya majira, angaliwe kwa karibu kuhakikisha matatizo hayo ya kiafya yasizidi. Kama hakuna mabadiliko, basi ni bora kuendelea kutumia vidonge mseto vya majira. Kama matatizo yataongezeka, asimamishe mara moja kutumia vidonge hivyo haraka.

   

  Kidonge kidogo chenye projestini tu

  Kidonge hiki cha majira hakina homoni ya estrojeni, kina projestini tu. Ni salama kwa wanawake wengi ambao hawawezi kutumia vidonge mseto vya majira na vina madhara ya pembeni kidogo kuliko vidonge mseto. Kidonge kidogo cha majira hakipunguzi maziwa kwa wanawake wanaonyonyesha. Wanawake wanaotumia kidonge kidogo wanaweza kupata mabadiliko katika tarehe za hedhi, damu kidogo kati ya kipindi cha hedhi kimoja na kingine, au kukosa hedhi kabisa.

  Vidonge vyote kwenye paketi ya vidonge vidogo vya majira vina kiwango sawa cha homoni. Tumia kidonge 1 kila siku.

  Jinsi ya kutumia kidonge kidogo cha majira

  Tumia kidonge chako cha kwanza kwenye siku yako ya kwanza ya hedhi. Halafu tumia kidonge kimoja muda huo huo kila siku, hata kama hutafanya tendo la ngono. Utakapomaliza paketi, anza paketi mpya siku inayofuata, hata kama hujapata damu yotote. Usiruke siku. Kila kidonge kina kiasi sawa cha homoni ya projestini.

  Kama utatumia kidonge kidogo hata baada ya kuchelewa saa chache, au kama utasahau kidonge cha siku 1, unaweza kupata mimba. Kama utakosa kutumia kidonge, kitumie haraka mara utakapokumbuka. Halafu tumia kidonge kinachofuata katika muda ule wa kawaida, hata kama itamaanisha kutumia vidonge 2 katika siku moja. Tumia kondomu au usifanye ngono kwa siku 7. Unaweza kutokwa na damu kidogo kama hutatumia kidonge chako kidogo au unapokitumia ukiwa umechelewa.

   

  Madhara ya pembeni ya vidonge vidogo vya majira

  Madhara ya kawaida kwa vidonge vyenye homoni moja ya projestini (vidonge vidogo) ni mabadiliko katika mpangilio wa hedhi ya kila mwezi. Unaweza kupata damu wakati hutarajii. Hedhi inaweza kutopatikana kabisa. Hii siyo hatari. Madhara mengine yanaweza kujumuisha kuongezeka uzito, kuumwa kichwa, na vipele vidogo mwilini.

  Dawa zinazoingiliana na kidonge kidogo cha majira

  Rifampicin (dawa ya kifua kikuu), ritonavir (dawa ya VVU) na baadhi ya dawa za kifafa huathiri utendaji wa vidonge vya majira. Kama utatumia dawa hizi, chagua njia tofauti ya uzazi wa mpango. Wanawake wanaotumia insulini kwa ajili ya kisukari wanaweza kuhitaji kurekebisha kiasi cha insulini baada ya kuanza kutumia vidonge vya majira.

  Kusitisha matumizi ya vidonge vidogo vya majira

  Kama unataka kupata mimba au kubadilisha njia ya kuzuia mimba, unaweza kuacha kutumia vidonge vidogo vya majira wakati wote. Unaweza kupata mimba mara baada kusimamisha vidonge hivyo. Kama unataka kuepuka mimba, anza njia nyingine mara moja.

  Njia ya vijiti na sindano za kuzuia mimba

  Kama kilivyo kidonge kidogo cha majira, njia ya vijiti na sindano za kuzuia mimba vina homoni ya projestini tu, lakini mwanamke hatakiwi kukumbuka kutumia kidonge kila siku. Njia ya vijiti na sindano za majira ni rahisi kutumiwa kwa siri. Hata hivyo, siyo njia ya vijiti wala sindano za majira ambayo inatoa kinga dhidi ya maambukizi yanayopitia ngono vikiwemo VVU.

  Jinsi ya kutumia njia ya vijiti au sindano za majira

  Vijiti vya majira ni virija vidogo vya plastiki ambavyo mfanyakazi wa afya huingiza chini ngozi ya upande wa ndani wa mkono wa mwanamke. Huzuia mimba kwa miaka 3 hadi 5, kutegemea na aina ya vijiti.

  Sindano za majira hutolewa na mtaalam wa afya, mara moja kila mwezi 1, 2, au 3, kutegemea na aina ya sindano.

  Vijiti na sindano za majira ni njia rahisi kutumika kwa siri, na mwanamke hatakiwi kukumbuka kutumia kidonge kila siku. Vijiti vyote vya majira na baadhi ya sindano zina projestini tu. Aina moja ya sindano (sindano ya kila mwezi) ina homoni zote mbili –estrojeni na projestini. Hivyo sindano hii haifai kwa wanawake ambao hawawezi kutumia vidonge mseto vya majira. Mwanamke anaweza kuamua kusimamisha sindano za majira au kuondoa vijiti vya majira kama atataka kupata mimba. Njia ya vijiti au sindano haiwezi kutoa kinga yoyote dhidi ya maambukizi yanayopitia ngono vikiwemo VVU.

  Madhara ya pembeni

  Sindano za majira za kila mwezi zinaweza kuwa na madhara ya pembeni yanayofanana na vidonge mseto vya majira. Njia ya vijiti na sindano za projestini tu zina madhara ya pembeni yanayofanana na vidonge vidogo vyenye projestini tu. Madhara hayo ni kama vile:-

  -Mabadiliko katika hisia kama vile kuhisi huzuni au kuudhika kwa urahisi

  -Maumivu ya Kichwa,

  -Kutokwa na damu kidogo katikati ya vipindi vya kawaida vya hedhi,

  -Matiti kuvimba na kuuma,

  -Kichefuchefu

  Dawa ambazo huingiliana na njia ya vijiti na sindano za majira

  Rifampicin (dawa ya kifua kikuu) na baadhi ya dawa za kifafa hupunguza ufanisi wa njia ya vijiti na sindano za majira. Kama unatumia dawa hizi, tumia njia tofauti ya uzazi wa mpango. Wanawake ambao wanatumia insulini kwa ajili ya tatizo la kisukari wanaweza kuhitaji kurekebisha kiasi cha insulini wanachotumia baada ya kuanza njia ya vijiti au sindano za majira.

  Kusitisha matumizi ya vijiti au sindano za majira

  Ili kusitisha matumizi ya vijiti, unapaswa kupata mtaalam wa afya ambaye ataviondoa. Mwanamke anaweza kupata mimba mara moja baada ya kuondoa vijiti hivyo vya majira. Kusimamisha sindano za majira ni rahisi. Ni suala la kuacha kuchoma sindano hizo. Inaweza kuchukua muda mrefu zaidi kwa mwanamke kupata mimba baada ya kusimamisha matumizi ya sindano za kuzuia uzazi. Hata hivyo wanawake wengi wanaweza kupata ujauzito ndani ya mwaka 1.

  Njia ya kitanzi

  Kitanzi cha kuzuia uzazi ni kidude kidogo cha plastiki, au plastiki na shaba, ambacho huwekwa kwenye kizazi cha mwanamke na mtaalam wa afya. Kitanzi huzuia mbegu za kiume kurutubisha yai la uzazi, na pia huzuia yai kutojibanza kwenye ukuta wa tumbo la uzazi.Njia ya kitanzi ina kiwango kikubwa cha ufanisi, na kitanzi kinaweza kukaa ndani ya kizazicha mwanamke kwa muda kuanzia miaka 5 hadi 12, kutegemea na aina ya kitanzi. Kitanzi hakitoi kinga dhidi ya maambukizi yanayopitia ngono vikiwemo VVU.

  Kitanzi ni njia salama kwa wanawake ambao wamewahi kupata ujauzito na wale ambao hawajawahi kupata mimba. Kitanzi kinaweza kuingizwa kwenye kizazi cha mwanamke wakati wote ule anapokuwa hana ujauzito, na akiwa hana maambukizi ukeni au maambukizi yanayopitia ngono. Kitanzi kinaweza pia kuondolewa na mtalaam wa afya wakati wowote ule. Baada ya kuondolewa, mwanamke anaweza kupata mimba bila kuchelewa.

  Mara baada ya kuingizwa kwenye kizazi, siyo rahisi kitanzi kutoka lakini inawezekana. Mara moja kwa mwezi, unaweza kukagua kama kamba za kitanzi ambazo huninginia kutoka kwenye mlango wa kizazi bado zipo kwa kuingiza kidole ndani ya uke wako na kuzigusa (lakini siyo kuzivuta). Kama huwezi kuzigusa au kama unafikiri kitanzi kimetoka, tumia kondomu au epuka kufanya ngono hadi utakapopata uchunguzi wa mtaalam wa afya.

  Madhara ya pembeni ambayo yanaweza kutokea kutokana na matumizi ya njia ya kitanzi

  Madhara ya pembeni ya kawaida ni hedhi kuwa nzito zaidi, ikiambatana na maumivu zaidi kuliko kawaida. Hali hii inaweza kuumiza lakini siyo hatari na taratibu hupungua baada ya miezi michache. Baadhi ya aina za vitanzi vina homoni ya projestini, ambayo husaidia kupunguza kero na damu ya hedhi. Kitanzi chenye projestini kinaweza kusababisha madhara ya pembeni yanayofanana na ya vidonge vidogo vya majira.

  Nani hapaswi kutumia kitanzi

  • Wanawake wenye saratani ya mlango wa kizazi au tumbo la uzazi. Wanawake wenye saratani ya matiti hawapaswi kutumia kitanzi chenye projestini, lakini wanaweza kutumia kwa usalama kitanzi chenye shaba.
  • Wanawake wanougua kisonono, klamidia, au maambukizi sehemu ya nyonga (kwenye kinena). Kwa taarifa zaidi juu ya ugonjwa wa kisonono na klamidia, angalia Matatizo na maambukizi sehemu za ukeni na umeni (kinaandaliwa).

Je Ungependa Kupokea Makala Zetu? Jiunge sasa ili kuweza kuzipata makala Zetu kila Mwisho wa Wiki moja kwa moja kwenye simu yako!

* inahitajika 


AdvertisementMtokambali 728x90